dc.description.abstract | Vikatuni vina wajibu muhimu katika aushi ya watoto na vijana ulimwenguni. Huenda
ndio sababu Karne ya 21 imeshuhudia ongezeko la tafiti kuhusu vikatuni. Utafiti huu
ni Uchanganuzi Makinifu wa Diskosi katika Vikatuni vya Shujaaz. Malengo ya utafiti
yalikuwa: Kueleza namna muwala ulivyokuzwa katika vikatuni vya Shujaaz.
Kufafanua mikakati ya mazoeaya kijamii katika vikatuni vya Shujaaz na kutathmini
jinsi mahusiano ya uwezo yalivyowasilishwa katika vikatuni vya Shujaaz. Nadharia
iliyoongoza utafiti huu ni nadharia ya Uchanganuzi Makinifu wa Diskosi. Maazimio
ya nadharia hii ni kuwa matumizi ya lugha katika jamii huchukuliwa kuwa mchakato
wa jamii. Lugha si zao la jamii tu bali ni nguvu muhimu katika kuunda michakato
iliyo chanya au hasi. Mojawapo ya madhumuni ya nadharia ya Uchanganuzi Makinifu
wa Diskosi ni kusaidia katika uchanganuzi wa diskosi ili kufichua imani za kiitikadi
zinazochukuliwa kuwa za kweli na kukubaliwa katika jamii. Data ya utafiti huu
ilitokana na sampuli ya nakala 35 zilizoteuliwa kimakusudi kwa kuzingatia
uchanganuzi wa yaliyomo kwa mujibu wa maswali ya utafiti. Utafiti ulichukua
muundo wa utafiti wa kimaelezo. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa njia ya
udondoaji matini iliyojumuisha maandishi na michoro ya picha. Uchanganuzi wa data
na matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo. Matokeo yaliashiria kuwa
muwala hukuzwa na: mada, sauti za kionomatopeya, maandishi katika mandhari ya
paneli, maelezo ya mwandishi na uzungumzi nafsi. Muwala uliokuzwa ni wa aina ya;
mada, msuko na muwala wa kijumla. Unominishaji, jazanda, ujumlishaji, utata wa
maana, deiksisi za nafsi ndio mikakati ya mazoea ya kijamii yaliyotumika kuwasilisha
diskosi ya Shujaaz. Hatimaye, mahusiano ya uwezo yaliwasilishwa kupitia kwa
wahusika, wahusika na vijana, wadhamini na vijana, hadhira na mtu mashuhuri na
mahusiano ya uwezo baina ya uana. Utafiti huu unatoa mchango wa kiisimu kwa
kufasiri lugha teule kama mkakati wa kuwashurutisha na kuwawekea vizingiti vijana
ili kuwadhibiti. Pili, kufafanua mikakati iliyotumiwa na wenye uwezo ili
kujitambulisha na vikundi maalumu katika jamii hasa vijana nchini Kenya. Utafiti huu
unapendekeza kuwa tafiti za baadaye zifavywe katika Shujaaz kwa kuzingatia
masuala ibuka, majukumu ya sauti ya kionomatopeya kando na kukuza muwala na
naratolojia. | en_US |