UKIUKAJI WA HAKI ZA WATOTO KATIKA RIWAYA YA CHOZI LA HERI
Abstract
Lengo la makala haya ni kubainisha ukiukaji wa haki za watoto katika riwaya ya Chozi la Heri (Matei, 2017). Ni vyema ikaeleweka kwamba tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili. Yaani watoto wa kiume sambamba na wale wa kike. Data ya utafiti huu imepatikana maktabani kwa kusoma riwaya teule kisha ikachanganuliwa kwa misingi ya Nadharia ya Uhalisia kwa mujibu wa Ntarangwi (2004) na lengo la makala. Nadharia hii inasisitiza kuwa kazi za sanaa zinapaswa kujikita katika kuusawiri ulimwengu kama ulivyo wala si kama unavyofikiriwa kuwa. Makala haya yamebainisha kuwa katika riwaya ya Chozi la Heri (Matei, 2017) ukiukaji wa haki za watoto upo kwani kuna mauaji ya watoto, ulanguzi wa watoto, kutoshughulikiwa kiafya, kuwepo kwa watoto mitaani, ajira ya watoto, watoto kushiriki katika ulanguzi wa dawa za kulevya na utumiaji wa mihadarati. Isitoshe, imebainika wazi kwamba kuna ukiukaji wa haki za watoto kupitia upashwaji tohara kwa wasichana, ukosefu wa mapenzi ya wazazi na dhuluma za kimapenzi. Kulingana na Nadharia ya Uhalisia, hii ni picha ya yale yanayowatendekea watoto katika jamii ya sasa. Mtafiti anapendekeza kuwa haki za watoto zinahitaji kutiliwa maanani na kila mja yeyote katika jamii. Hawa ndio viongozi wa kesho na iwapo wataathirika wakiwa wachanga basi kutakuwepo na changamoto za adinasi wa kutegemewa katika jamii.