UHALISIA WA KIMANDHARI NA KIMAUDHUI KATIKA RIWAYA YA SIKU NJEMA (1996)
Abstract
Kulingana na Ntarangwi (2004), fasihi huwakilisha maisha kwa upana wake na hasa uhalisi wa kijamii. Aidha, anasema kuwa mojawapo ya majukumu muhimu ya fasihi ni kuwasaidia wanadamu kuyaeleza vyema masuala wanayokumbana nayo kibinafsi na pia kama jamii. Isitoshe, fasihi ni chombo kinachoisaidia jamii kujielewa na kuyaelewa mazingira yake. Basi, lengo la makala haya ni kubainisha uhalisia uliopo wa kimandhari na kimaudhui katika riwaya ya Siku Njema (1996). Makala haya yametumikiza nadharia ya Uhalisia ili kubainisha uhalisi uliopo wa kimandhari na kimaudhui katika riwaya husika. Data ya makala haya ilipatikana kwa kusoma riwaya husika kisha ikachanganuliwa kwa misingi ya malengo na nadharia teule. Matokeo ya uchunguzi yamethibitisha kwamba kuna uhalisi wa kimandhari na kimaudhui katika riwaya ya Siku Njema (1996) kwa sababu majina ya mazingira yanayozungumziwa na mwandishi yanapatikana katika Afrika Mashariki hususan nchini Uganda, Tanzania na Kenya. Isitoshe, maudhui yaliyoangaziwa na mwandishi yana ukuruba na masuala yanayoikabili jamii ya leo. Mwandishi anaonekana kuathiriwa na mazingira yaliyomzunguka pamoja na matukio ya jamii yake ya karibu. Hii ni ishara kuwa kazi yake haijabuniwa kutoka katika ombwe tupu. Dhihirisho kwamba, fasihi ni picha halisi ya jamii.