dc.description.abstract | Unyambulishaji wa vitenzi ni mojawapo ya masuala yanayoshughulikiwa katika
taaluma ya mofolojia katika lugha nyingi za Kiafrika. Mofolojia ni tawi la isimu
linaloshughulikia umbo la ndani la neno ambalo hujishughulisha na unyambulishaji
wa vitenzi. Vitenzi ni maneno ambayo lazima yawepo katika sentensi ili ikamilike
kimaana. Utafiti huu umeshughulikia unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ kwa
malengo ya kufafanua mifanyiko inayohusika katika utaratibu wa unyambulishaji wa
vitenzi katika Kigĩchũgũ na kutathmini kanuni zinazoruhusu au kuzuia mifanyiko
hiyo ya unyambulishaji. Katika uainishaji wa Guthrie, Kigĩchũgũ ni mojawapo ya
lugha za Kiafrika ambayo hudhihirisha unyambulishaji. Kigĩchũgũ kinawekwa katika
kundi la E hasa katika E51 linalojumuisha lugha za Kibantu ambazo zimeimarika
katika mofolojia ya uundaji na unyambulishaji wa vitenzi. Utafiti huu uliongozwa na
mihimili ya nadharia ya Mofolojia Leksia iliyoasisiwa na Kiparsky na kuendelezwa
na Katamba na Stonham, yaani mihimili ya Ngazi Leksia, Kufuta Mabano, Kuhifadhi
Muundo, Kwingineko na Mzunguko Sheria. Nadharia ya Mofolojia Leksia ni
nadharia zalishi na nyambulishi. Nadharia ya Mofolojia Leksia huonyesha uhusiano
wa sheria zinazojenga maumbo ya kimofolojia na sheria zinazodhibiti namna
maumbo haya yanavyotamkwa. Kanuni ya Kioo kwa mujibu wa Baker pia iliongoza
utafiti huu kwani inaeleza kuwa unyambulishaji wa vitenzi katika lugha za Kibantu
hufuata mpangilio maalum wa unyambulishaji. Data ya sampuli ya vitenzi vya
Kigĩchũgũ ilitumika katika utafiti ambapo mtafiti alizalisha kimaksudi vitenzi sitini
(60) kutokana na sentensi za Kigĩchũgũ ambavyo vilitumika katika utafiti kwa kuwa
ana uelewa na umilisi wa Kigĩchũgũ. Mtafiti alienda nyanjani katika kata za Kabare,
Baragwi, Karumandi, Ngariama na Njukini. Kata hizi zilichaguliwa kimaksudi kwani
zina wazungumzaji halisi wa Kigĩchũgũ. Vitenzi hivi viliwekwa katika kauli sita za
unyambulishaji na kuainisha mifanyiko inayohusika katika utaratibu wa
unyambulishaji kwa kutumia jedwali la mnyambuliko wa vitenzi. Maana
zinazowakilishwa na maumbo ya unyambulishaji pia zilijadiliwa. Matokeo ya utafiti
yalionyesha kuwa Kigĩchũgũ ni lugha ambishi kwani huchukua viambishi awali na
tamati. Upachikaji wa viambishi tamati katika vitenzi vya Kigĩchũgũ ulichangia
katika kuongeza maana za vitenzi. Matokeo ya utafiti pia yalionyesha kuwa
Kigĩchũgũ hukubali mifuatano ya viambishi nyambulishi viwili, vitatu na hata vinne.
Matokeo ya utafiti huu yatachangia katika kuongeza maarifa ya kiutafiti yanayohusu
sarufi ya Kigĩchũgũ. Aidha, yatasaidia kuhifadhi Kigĩchũgũ kama mojawapo ya lugha
za Kiafrika katika maandishi. Utafiti pia utachangia katika kuwanufaisha watafiti wa
baadaye watakaoshughulikia Kigĩchũgũ. | en_US |