dc.description.abstract | Ulinganifu, usahihi pamoja na uwazi ni vipengee muhimu vya kuchunguzia kazi za fasihi tafsiri. Utafiti huu ulilenga kutafiti ulinganifu katika mtiririko wa kazi mbili teule za Kimenye (1968): Moses in Trouble na Moses and the Ghost zilizotafsiriwa ili kubainisha umuhimu wa kutumia mikakati mwafaka ya kutafsiri tamathali za usemi na nomino za pekee ili kupata tafsiri wasilifu. Utafiti huu ulijibu maswali kuhusu mikakati iliyotumiwa kutafsiri tamathali mbalimbali ili kubainisha ulinganifu katika tafsiri za Matundura (2013): Musa Mashakani na Musa na Pepo na kuhusu ulinganifu na usahihi katika tafsiri za nomino za pekee katika tafsiri za Musa Mashakani na Musa na Pepo. Katika kuyajibu maswali haya, mifano ilitolewa kutoka kwenye tafsiri za Matundura (2013): Musa Mashakani na Musa na Pepo na matini zake za Kiingereza za Kimenye (1968): Moses in Trouble na Moses and the Ghost. Msururu wa Musa uliteuliwa kwa kuwa umeandikwa na mwandishi mmoja na kutafsiriwa na mtafsiri mmoja. Kwa hivyo kuna uthabiti kwa upande wa mwandishi na mtafsiri. Aidha, huu ndio msururu wa pekee kuwahi kutafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza hadi Kiswahili. Sababu ya kuteua Musa Mashakani na Musa na Pepo ni kuwa kazi hizi zimesheheni tamathali za usemi na hivyo mtafiti alitazamia kupata data ya kutosha kuweza kuafikia madhumuni ya utafiti. Aidha kazi hizi hazijafanyiwa utafiti. Nadharia ya Ulinganifu ilitumiwa kuchunguza matini mbili za Kimenye (1968) zilizoteuliwa kama kielelezo. Utafiti huu ulifanyika maktabani. Data ilichanganuliwa kwa mbinu elezi kwani ilikuwa data ya nathari. Sampuli ilikuwa vitabu vinne vilivyoteuliwa kuwakilisha vingine: viwili vilivyoandikwa kwa Kiingereza na tafsiri zao za Kiswahili. Uteuzi huu ulifanywa kimakusudi kwa kuwa msururu mzima una wahusika walewale, mandhari haibadiliki ila matukio tu ndiyo tofauti. Vifaa vilivyotumika kukusanyia data kutoka kwa sampuli vilikuwa matini mbili za Kimenye (1968): Moses in Trouble na Moses and the Ghost pamoja na tafsiri zao za Matundura (2013): Musa Mashakani na Musa na Pepo. Utafiti huu uligundua kwamba mikakati ya kutafsiri tamathali za usemi hutumiwa kimwingiliano ili kuweza kuhamisha ujumbe usio na dosari. Ilibainika pia kuwa mikakati inayotumika kutafsiri nomino za
pekee kutoka lugha ya Kiingereza hadi Kiswahili hutegemea mchango wa nomino husika katika matini. Matokeo ya utafiti huu yataifaidi taaluma ya fasihi tafsiri kwa kuwapa wasomi wa tafsiri mwongozo wa kurejelea watakapokuwa wakifanya tafiti zao. Vilevile matokeo ya uchunguzi huu yatakuwa muhimu kwa watafsiri chipukizi kwa kuwapa mwongozo kuhusu mikakati ya kutafsiri tamathali za usemi hasa istiari, tashbihi na nahau. | en_US |